Search This Blog

Wednesday, April 25, 2018

ELIMU YA UFUGAJI WA KUKU.



DARASA LA UFUGAJI WA KUKU
LISHE BORA ENDELEVU KWA MATOKEO BORA ZAIDI
Mfugaji ili uwape kuku wako lishe bora yenye kuendelea, na ili upate matokeo bora zaidi katika ufugaji wako wa kuku basi yakupasa kuzingatia yafuatayo:

  • Tumia chakula bora na siyo bora chakula. Tumia chakula bora ambacho hakina madhara kwa kuku wako na hata walaji kwa ujumla.
  • Weka chakula mahali safi na salama kuepuka wadudu waharibifu kama vile panya ili kuzuia maambukizi ya magonjwa kwa kuku.
  • Tumia kanuni ya "least cost combination" yaan tumia chakula cha bei nafuu kinachotoa matokeo bora zaidi ili kupunguza gharama za ufugaji hali ambayo itakufanya upate faida mara dufu.
Kwa kufanya hivyo utaweza kuwalisha kuku wako chakula kilicho bora kwa matokeo bora zaidi bila kuyumba kiuchumi wakati wote wa ufugaji wako.
KUTUNZA KUMBUKUMBU KATIKA UFUGAJI
Kuna usemi usemao "mali bila daftari hupotea bila habari" ukiwa na mradi wowote wa ufugaji ni vema ukiwa unaweka kumbukumbu za kila siku au kwa kila wiki. Katika kutunza kumbukumbu za ufugaji kuna mambo muhimu ya kuyazingatia kama ifuatavyo:-

1. KUMBUKUMBU ZA KUKU NA UZALISHAJI
Hii ni kuanzia unapowapokea hadi kuwatoa bandani. Hapa unapaswa kila siku uwaangalie kuku wako ili kujua wanahali gani na ni wangapi waliopo, hapo utaelewa kama kuna ugonjwa wa kutibu au tahadhari gani zichukuliwe.
kama ni kuku wa mayai basi kujua idadi ya mayai wanyotaga kila siku, ili uweze kujua asilimia za utagaji na uweze kupima kiwango chao cha utagaji.

2. KUMBUKUMBU ZACHANJO
Weka kumbukumbu za chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali kama vile mdondo (Newcastle), gumboro, ndui na magonjwa mengine.

3. KUMBUKUMBU ZA  AFYA
Hapa unarekodi kila aina ya ugonjwa uliotekea bandani, idadi ya walioathirika, waliotibiwa, waliopona na waliokufa. Gharama za matibabu nazo pia ziwekwe kwenye kumbukumbu.

4. GHARAMA ZA VIFAA NA CHAKULA
Vifaa vyote unavyonunua kwa ajili ya ufugaji ni lazima viorodheshwe na viwekwe kwenye kumbukumbu, na gharama za chakula kuanzia unapoingiza kuku hadi unapowatoa iwekwe kwenye kumbukumbu pia.

MUHIMU: Njia rahisi ya kutunza kumbukumbu ni kununua daftari na kutengeneza majedwali yanayoonesha vipengele tajwa hapo juu.
ZINGATIA HAYA ILI UPATE FAIDA ZAIDI
Baada ya kuwa mfugaji amefuata taratibu zote katika ufugaji wake wa kuku kwa lengo la kupata faida, ili mfugaji huyo apate faida zaidi kuna mambo muhimu ya kuzingatia hususan katika kujenga soko lake kama ifuatavyo:-


1. Lenga soko sikukuu za mwisho wa mwaka na zinginezo ambapo kuku huuzwa zaidi.
2.Tafuta masoko ili ujenge jina kwa wanunuzi wakubwa.
3. Jiunge au shirikiana na wenzako kuunda kikundi cha wafugaji (wafuga kuku) ili muweze
  • Kuchanja pamoja kupunguza gharama (kwa wafugaji wadogo)
  • Kutafuta masoko pamoja
  • Kupasiana wateja kama hauna kuku wakati huo
4. Kuweza kujitambulisha katika masoko kwamba Kijiji au kikundi chenu kuku wanapatikana muda wote

FIKIRIA KIKUBWA ANZA NA KIDOGO
Hii ni kwa wote, wafugaji na wanaotaka kuanza kufuga. Unapotaka kuanza ufugaji unatakiwa uanze na ufugaji mdogo hatakama una mtaji mkubwa. Kwa kufanya hivi itakusaidia kupata uzoefu katika nyanja zifuatazo:

1. UTUNZAJI (MANAGEMENT)
Kwa kuanza na kiasi kidogo itakusaidia kujua ni ukubwa gani unafaa kwa kuku wangapi, ukiwa na kuku wangapi utalisha chakula kiasi gani, pia utapata uzoefu wa chanjo muhimu zinazohitajika hali ambayo itakurahisishia pindi utapoanza ufugaji mkubwa.

2. SOKO
Hapa tunalenga upatikanaji wa wateja wa bidhaa zako za mifugo, itakusaidia kujua wateja waliopo wanavutiwa na bidhaa ya aina gani, kwa mfano mayai utajua wanapenda mayai ya kiini cheupe au cha njano? Kwa kufaham wanchokihitaji utajua ufanye nini ili ukidhi wanachokihitaji.

3. CHANGAMOTO
Ukianza na ufugaji mdogo pia itakusaidia kujua changamoto zilizopo kwenye ufugaji na utajifunza ni jinsi gani ya kuzitatua au kukabiliananazo kabla  ya kuanza ufugaji mkubwa.
MAZOEA YANAYOWAGHARIMU WAFUGAJI
Kuna baadhi ya wafugaji huwa wanafuga kwa kutegemea uzoefu walionao katika ufugaji bila ya kujali kuwa kuna mabadiliko kila siku katika sekta ya mifugo, wengi wao huwa wanatatua kesi mbalimbali zinazotokea katika ufugaji kwa kutumia uzoefu hali ambayo inawasababishia kupata hasara kubwa isiyo ya lazima. Yafuatayo ni baadhi ya mazoea yanayowagharimu wafugaji:-

1. KUINGIZA VIFARANGA BILA MAANDALIZI SAHIHI
Wengi wa wafugaji huwa wanaingiza vifaranga pasipo kufuata utaratibu wa kitaalam katika kuandaa banda pamoja na maandalizi ya kupokea vifaranga. Na kama atabahatika kufanya usafi basi atafanya juujuu tu hali ambayo inasababisha banda kuhifadhi vimelea vingi vya magonjwa na kupelekea kuku kuugua na kufa kuanzia wanaingia hadi kufikia kuuzwa, na hatimaye mfugaji hupata hasara kwani hutumia pesa nyingi kwenye madawa kwa kutibu na pesa nyingi kwenye chakula kwa kuchelewa kukua kutokana na kuumwa.

2. KULISHA BILA KUFUATA MAELEKEZO SAHIHI
Kila aina ya kuku wanautaratibu wa ulishwaji chakula, utaratibu ambao ukikiukwa huwezi kupata matokeo mazuri ya mifugo yako, ila wafugaji wengi huwa wanalisha kwa utaratibu usio sahihi ambao wao wanadhani kwamba ndio wataongeza uzalishaji wa mayai au watakuwa haraka kwa upande wa kuku wa nyama, na kuna wengine wanadiriki kutumia chakula aina moja mwanzo mwisho, yaan anaweza kutumia chakula cha vifaranga wa nyama (SUPER STARTER) kuanzia mwanzo hadi anauza kuku bila kufaham kwamba kila aina ya chakula ina kazi yake katika kila hatua ya umri. Lakini pia bila kujali kwamba analisha kwa gharama kubwa hali ambayo itampunguzia faida.

3. KUTIBU KWA DAWA AMBAYO SI CHAGUO KWA UGONJWA HUSIKA
Kama inavyofahamika kuwa wafugaji wa kuku wengi wamebarikiwa kwa kufaham majina mengi ya dawa za kuku, na kwa kutumia uzoefu walionao huwa wanatibu kuku wao magonjwa mbalimbali bila kupata maelekezo kutoka kwa Dokta au Mtaalam wa mifugo. Kwa kufanya hivyo hutumia dawa nyingi tofautitofauti kwa kutibu ugonjwa mmoja bila mafanikio na kupelekea ugonjwa kuwa sugu na idadi ya vifo kuongezeka siku hadi siku.

USHAURI: Sio kila mfugaji mzoefu anaweza kuwa Daktari, ila kila Daktari anaweza kuwa mzoefu.
MBINU ZA KUKINGA KUKU DHIDI YA MAGONJWA
Tunafahamu kwamba magonjwa ndio chanzo kikubwa cha kukatisha ndoto za mfugaji kutokana na ughali wa bei za dawa au vifo vinavyosababishwa na magonjwa hayo. Lakini upo uwezekano wa kuyaepuka hayo ikiwa tutazingatia yafuatayo kwa uangalifu mkubwa:-
  • Chanja kuku dhidi ya magonjwa mbalimbali yasiyotibika kama vile mdondo, gumboro na ndui.
  • Usifuge kuku na ndege wengine kama vile bata, kanga au kwale katika banda moja. Pia usichannganye kuku wa asili na wa kisasa katika banda moja, yaan kwa mfano usichanganye kuku wa nyama(broilers) na kuku wa asili.
  • Usirudishe nyumbani kuku waliopelekwa sokoni wakakosa soko kwani wanaweza kuleta magonjwa.
  • Ondoa kuku wote wenye dalili za ugonjwa na uwatibu kwa dawa husika, na waliokufa wazike au wachome moto.
  • Watenge kuku wageni kwa takribani wiki mbili kabla ya kuwachanganya na wa zamani.
  • Usafi wa banda, vyombo vya maji na kulishia, na muhudumu ni vya kuzingatia pia.
  • Zuia watu wasiohusika, au ndege kuingia au kukaribia banda.
  • Kuwepo mavazi na viatu maalum vya kuingilia bandani.
  • Mlangoni kuwekwe dawa ya kuulia vijidudu kwa ajili ya kukanyaga kabla ya kuingia bandani.
  • Banda lipumzishwe wiki mbili kabla ya kuingiza kuku wapya.
  • Wape kuku chakula bora na maji safi na salaama. Maji safi na salaama ni yale ambayo hata wewe mfugaji unaweza kuyanywa.
KANUNI ZA KUONGEZA FAIDA KATIKA UFUGAJI KUKU
Ufugaji kuku ni biashara kama biashara nyingine, kuna wafugaji wengi wanaingia gharama zisizo za lazima katika kufuga kuku hali ambayo inawapelekea kupunguza faida yao na maranyingine hata kutopata faida kabisa, hali hii inawakwaza wafugaji na wengine hukata tamaa kabisa ya kufuga. Lakini hayo yanasababishwa na wao wenyewe wafugaji bila wenyewe kujijua.
Kupitia somo hili tutakumbushana ni namna gani mfugaji anaweza kuzikwepa gharama zisizo za lazima katika ufugaji ili aweze kupata faida mara dufu. Zifuatazo ni kanuni za kuongeza faida katika ufugaji kuku:-

1. KUPATA VIFARANGA BORA
Vifaranga bora ni wale waliototolewa katika wakati uliopendekezwa kitaalaam hali ambayo inamjenga kifaranga kuwa na kinga asilia ya mwili ya kutosha, kwahiyo mfugaji anaweza kufuga hadi kufikia kuuza bila kutumia dawa za kutibu ugonjwa wowote zaidi ya chanjo na dawa za kuanzishia tu, hivyo ataokoa pesa nyingi za kumuita daktari na kununua madawa na faida itaongezeka siku hadi siku.

2. ULEAJI MZURI (PROPER MANAGEMENT)
Hapa tunakusudia uasafi wa banda, vyombo vya chakula na maji, maji ya kunywa na muhudumu mwenyewe. Kwan magonjwa mengi ya kuku yanasababishwa na uchafu, hivyo uleaji ukiwa mzuri magonjwa hayatakuwepo halikadhalika na na gharama za matibabu hazitakuwepo pia.

3. CHAKULA BORA
Mfugaji anatakiwa ahakikishe anapata chakula bora kwa ajili ya kuku wake, chakula bora ni ambacho kimekingwa na magonjwa yote na kinakuza kuku kwa wakati, lakin pia chakula bora ni kile ambaho hakisababishi mazingira hatarishi katika banda kama vile kulowesha banda. Chakula ambacho kinalowesha banda kina hatari ya kusababisha magonjwa mbalimbali kama vile coccidiosis na typhoid, hali ambayo mfugaji ataingia gharama za kutibu mara kwa mara na kununua maranda.

4. KUPATA SOKO LA UHAKIKA
Ili upate soko la uhakika ni lazima uwe na tabia ya kutafuta taarifa (search information), kwa kutafuta taarifa itakuwezesha kujua hali ya soko iliyopo ili nawe uweze kujipanga. Na kama ukiwa unategemea tu mtu wa tenga aje mara nyingi utakuwa unalalamikia soko, hali ambayo itakupa stress na kuuza kuku wako kwa bei ya hasara. Ila kama unajua hali halisi ya soko basi hata akija mtu wa tenga nyumbani hatokudanganya na utakuwa na uhakika na bei yako.

FAIDA ZA UFUGAJI KUKU
Tunafaham kuwa unajua faida za kuku lakini ngoja tukumbushe yafuatayo kuhusu faida za ufugaji kuku.
  • Kuku ni chanzo cha haraka cha pesa kwa kuuza kuku au mayai.
  • Kuku wanaweza kabisa kukuongezea kipato na kukuondolea kabisa umaskini.
  • Nyama ya kuku na mayai ni protini muhimu kwa familia, yaan watoto, wagonjwa na hata wazee.
  • Kinyesi cha kuku pia ni mbolea, lakini kama haitoshi maganda ya mayai na manyoya ni mapambo.
  • Hakuna dini wala utamaduni wowote Tanzania unaozuia kula kuku.
  • Katika nyama ambayo haina madhara yoyote katika mwili wa binadamu ni nyama ya kuku na samaki.
  • Ni mradi unaompa fursa kusimamia hata mwajiriwa bila kuathiri ajira yake.
  • Na kwa wale akina fulani katika shughuli za kijadi kuku ni moja ya zawadi au malipo kama mteja hana pesa.
MATATIZO YALETWAYO NA UPUNGUFU WA VITAMINI MWILINI (2)

VITAMINI D
Husaidia madini aina ya calcium na phosphorous kuchukuliwa na mwili ili kuimarisha mifupa na kutengeneza ganda la yai la kuku. Jua husaidia mwili wa kuku kutengeneza vitamini D.

Dalili za Upungufu wa Vitamini D Mwilini

  • Rickets: Mifupa huwa laini(soft), hupinda, magoti huvimba, na midomo huwa laini. Hii hutokana na madini aina ya calcium na phosphorous kutojengeka kwenye mifupa.
  • Maganda ya mayai huwa laini.
  • Kukua polepole.
  • Mayai hupungua.
  • Uanguaji hafifu wa mayai.


VITAMINI E
Dalili za Upungufu wa Vitamini E Mwilini

  • Ugonjwa uitwao "crazy chick" au "nutritional encephalomalacia" ambapo ubongo wa kuku huwa laini na kuathiri mishipa ya fahamu. Dalili zake ni:-
                   -Shingo hupinga
                   -Kifaranga huanguka kifudifudi
                   -Kichaa
  • Majike hupunguza utagaji wa mayai.
  • Mayai hayaanguliwi vizuri

VITAMINI K
Husaidia kuzuia kuvuja damu. Ikikosekana mwilini mishipa ya damu hupasuka na kusababisha damu kuvuja. Vitamini hii hupatikana katika alfalfa, samaki (fish meal) na nyama.

VITAMINI B1 (THIAMIN)
  • Huleta hamu ya kula.
  • Upungufu hufanya kichwa kurudi nyuma (Head retraction)
  •  Siyo rahisi kupata upungufu wa vitamini B1 mwilini kwa kuwa vyakula vingi vina vitamini hii.
  • Hupatikana katika nafaka, alfalfa na mafuta (oil).
Vitamini C
Husaidia kifaranga kilicho ndani ya yai kukua, mifupa ya kifaranga kuumbika na kukua vizuri, pia mafuta kusambaa vizuri mwilini.

Vitamini A
Huhitajika kwa kiwango kidogo sana katika chakula cha kuku, lakini kiasi hicho kidogo ni muhimu sana kwa kuku ili aweze kukua, kutaga mayai mazuri, mayai yaanguliwe vizuri na macho yaweze kuona vizuri.

Dalili za Upungufu wa vitamini A mwilini.
  • Kuku hukawia kukua.
  • Kuku huwa dhaifu na mwenye manyoya yasiyo na mpangilio.
  • Macho hayaoni vizuri.
  • Utagaji usioridhisha.
  • Mayai yatagwayo hayaanguliwi vizuri.
  • Mayai huwa na doa au madoa madoa ya damu ndani yake (blood spots in eggs)
  • Kukishwa kujikinga na maradhi ipasavyo.
  • Kukonda.
  • Manyoya hayaoti ipasavyo (poor feathering).    
  • ITAENDELEA